Takribani nusu (asilimia 48) ya wanawake na theluthi moja (asilimia 32) ya wanaume nchini wanaamini mume ana haki ya kumpiga mke au mwenza iwapo hatowahudumia watoto, atatoka nyumbani bila kumtaarifu, atabishana naye, atakataa kujamiiana au kuunguza chakula.
Hayo yameelezwa katika Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa Mwaka 2022 uliotekelezwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali (OCGS), Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara za Afya kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Katika idadi hiyo, asilimia 38 ya wanawake na asilimia 23 ya wanaume wametaja kutohudumia watoto kama sababu kubwa ya mwanaume kumpiga mkewe au mwenza wake.
Watanzania wengi huchukua hadi miaka 18 kumaliza kujenga nyumba
Aidha, utafiti umebaini asilimia 27 ya wanawake wa Tanzania wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wamewahi kufanyiwa ukatili wa kimwili tangu wakiwa na umri wa miaka 15. Katika kipindi cha miezi 12 iliyopita kabla ya utafiti huo, asilimia 18 ya wanawake walifanyiwa ukatili wa kimwili.
Utafiti umeeleza kuwa zaidi ya theluthi moja (asilimia 35) ya wanawake walioolewa au wanaoishi na wenza wa karibu wamewahi kufanyiwa ukatili wa kimwili, ikilinganishwa na asilimia 4 ya wanawake ambao hawajawahi kuolewa. Miongoni mwa wanawake walioachika, kutengana, au wajane, asilimia 50 wamewahi kufanyiwa ukatili wa kimwili.