Askari 17, maafisa wawili washikiliwa kwa kusababisha vifo vya watu wawili

0
38

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia na kuwahoji askari 11 wa kampuni ya ulinzi, maafisa wawili wa Wakala wa Huduma za Misitu pamoja na askari sita wa polisi kwa tuhuma za kuwajeruhi na kupelekea vifo vya watu wawili.

Kamanda wa Polisi Jumanne Muliro amesema tukio hilo limetokea Agosti 28 mwaka huu majira ya saa nane usiku Kiluvya wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam ambapo maafisa hao wakiwa katika majukumu yao ya kazi walikutana na kundi la watu takribani 30 waliokuwa wamepakia mikaa na kuwataka wasimame.

Ameongeza kuwa baada ya watu hao kulazimishwa kusimama na kukaidi waliacha pikipiki zao na kukimbia, baadaye walirudi wakiwarushia mawe maafisa hao na ndipo walipowafyatulia risasi ambazo zilipelekea kifo cha watu hao ambao bado hawajatambuliwa majina yao.

“Jeshi lilianza uchunguzi mara moja na kufuatilia kwa kina mazingira ya tukio lile na hasa kujikita katika vipengele vya matumizi ya nguvu, kutokana na mazingira ya kiuchunguzi ambayo bado unaendelea kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kiuchunguzi, watu hawa wamekamatwa, wamehojiwa kwa kina, na mamlaka zingine za uchunguzi zinaendela kufanya kazi,” ameeleza Muliro.

Aidha amesisitiza kuwa jeshi la polisi halitasita kufanya mwendelezo wa hatua za kisheria dhidi ya watu watakaobainika kuwa wamehusika kwa namna moja au nyingine kuvunja baadhi ya sheria wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Miili hiyo imehifadhiwa katika hospitali ya Mloganzila kwa ajili ya uchunguzi.

Send this to a friend