Askari aliyepandishwa cheo kwa kukataa rushwa milioni 10, avuliwa cheo hicho kwa kukutwa na hatia

0
14

Askari Polisi aliyepandishwa cheo na Mkuu wa Jeshi la Polisi kutoka Sajenti kuwa Stesheni Sajenti mwaka 2019 ameshushwa cheo na kurudi katika cheo alichokuwa awali.

Uamuzi wa kumshusha cheo Meshack Laizer aliyepandishwa cheo baada ya kukataa rushwa ya TZS milioni 10 umefikiwa baada ya kupatikana na hatia ya kukataa kuhudhuria mafunzo ya cheo kipya pasi na sababu ya msingi.

Laizer alitakiwa kuhudhuria mafunzo hayo kwa mujibu wa kanuni za jeshi hilo ili kumjengea uwezo wa kufanya kazi zinazoendana na ngazi ya cheo hicho.

Taarifa ya polisi imeeleza zaidi kuwa kutokana na kukataa amri halali ya Mkuu wa Jeshi la Polisi alishitakiwa kijeshi na kupatikana na hatia, na kwa mujibu wa kanuni baada ya kupatikana na hatia unatakiwa kushushwa cheo ngazi moja, na ndicho kilichofanyika.

Aidha, Mkuu wa Jeshi la Polisi ametoa karipio kali kwa Laizer ikiwa ni hatua  za awali wakati akisubiri hatua nyingine kufuata kwa mujibu wa taratibu za Jeshi la Polisi.

Mbali na kupandishwa cheo mwaka 2019, alipewa zawadi ya TZS milioni 1 kwa kukataa rushwa ya milioni 10 ili kuharibu ushahidi wa kesi aliyokuwa anaichunguza.

Send this to a friend