Askari Magereza ashikiliwa kwa tuhuma za kumuua mpenziwe kisa mapenzi

0
59

Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia na kumhoji Askari wa Jeshi la Magereza mwenye umri wa miaka 31 (jina limehifadhiwa) kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake, Bitie Chacha (25), mwalimu wa Shule ya Msingi, mkazi wa Bugweto A, Kata ya Ibadakuli, Manispaa ya Shinyanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amesema Bitie aliuawa juzi saa moja usiku kwa kuchomwa na kisu sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo mapajani, shingoni na kichwani.

Magomi amesema Bitie alikuwa akiishi na ofisa magereza huyo wakiwa ni wapenzi lakini walihitilafiana na ndipo mtuhumiwa akamshambulia mwalimu huyo.

Amesema Jeshi la Polisi limekuwa likitoa elimu kwenye jamii kuhusu malezi kwenye familia ili kadiri miaka inavyokwenda kisiwepo kizazi kinachofanya vitendo vya kikatili.

Aidha, mmoja wa rafiki wa Bitie (jina limehifadhiwa) amedai ugomvi wa wapenzi hao ulianzia baa baada ya askari huyo kuchukua simu ya mkononi ya Bitie na kusoma ujumbe mfupi.

Baadhi ya majirani wa wapenzi hao, wamedai mwalimu huyo alikuwa akiishi na mtuhumiwa na mara kwa mara walikuwa wakigombana.

Send this to a friend