Askari mgambo washikiliwa kwa tuhuma za wizi

0
106

Askari mgambo wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Lindi kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa mali mbalimbali, zikiwemo za raia mmoja anayeishi katika Manispaa ya Lindi.

Askari hao ni Karimu Athuman Omari (29), Askari Mgambo namba MG. 512421, mkazi wa mtaa wa Raha Leo, na Zawadi Swedi Mohamed (22), Askari mgambo namba MG. 624773, mkazi wa Mtanda, wote wakiwa wanatumikia kazi za ulinzi katika maeneo ya Manispaa ya Lindi.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na mali zinazodaiwa kuibwa kutoka kwa Anita Patel, mkazi wa eneo la Sokoine, pia walikutwa na mali nyingine zinazodhaniwa kuwa zimeibwa kutoka maeneo mengine tofauti.

Watuhumiwa hao baada ya kuhojiwa, walikiri kuhusika katika tukio hilo la wizi na kueleza kuwa walitekeleza wizi huo kutoka kwenye nyumba ya mlalamikaji, ambayo inapakana na nyumba ya mtumishi wa shirika la TANESCO, ambaye ndiye aliyekuwa akiwatumia kama walinzi wake binafsi.

Aidha, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi wote waliopotelewa au kuibiwa mali zao kufika Kituo Kikuu cha Polisi Lindi kwa ajili ya kutambua mali zao ambazo zimeokolewa katika msako huo.

Jeshi hilo limesisitiza kuwa uchunguzi unaendelea na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa wote watakaobainika kuhusika na matukio ya wizi au uhalifu wa aina yoyote ile.

Send this to a friend