Askari polisi auawa kwa mshale Loliondo

0
54

Askari Polisi mmoja ameuawa kwa kupigwa mshale wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wakati wa zoezi la uwekaji mpaka katika eneo la pori tengefu kwenye Tarafa ya Loliondo.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella akisema kwamba kifo hicho kilitokea Juni 10 alasiri, na kusisitiza kwamba kama serikali wanatambua uzalendo wa askari huyo.

Ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi wa Tarafa ya Loliondo wilaya ya Ngorongoro kuwa watulivu na kusikiliza maelekezo ya serikali katika zoezi la uwekaji mipaka.

Mongella ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama amesema hayo leo Juni 11, 2022 katika tarafa ya Loliondo wilaya ya Ngorongoro alipokuwa anaongea na vyombo vya habari kuhusiana na zoezi linaloendea la uwekaji mipaka katika wilaya hiyo.

Amesema kuna baadhi ya watu na mitandao ya kijamii inapotosha kuhusiana na kinachoendelea katika zoezi la uwekaji mipaka katika wilaya ya Ngorongoro.

Kwa mujibu wa sheria eneo la pori tengefu ni kilomita za mraba 4,000, lakini kwa kutambua umuhimu wa wanachi kati eneo hilo, serikali imepunguza pori tengefu hadi kilomita za mraba 1,500, huku 2,500 zikiachwa kwa ajili ya shughuli za wananchi.

Send this to a friend