Askari Polisi wapandishwa vyeo kwa kutoa huduma bora kwa Watalii.

0
52

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amewapandisha vyeo maofisa wawili wa Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha wanaofanya kazi katika kituo cha Polisi cha Utalii na Diplomasia baada ya kutoa huduma bora kwa watalii.

Waliopandishwa ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Waziri Tenga ambaye amepandishwa cheo kuwa Mrakibu wa Polisi (SP) na Mkaguzi wa Polisi (INSP), Anthony Mwaihoba  ambaye amepandishwa cheo kuwa Mrakibu Msaidizi wa Polisi  (ASP).

Masauni amechukua hatua  hiyo baada ya kupokea barua kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Italia iliyoandikwa na watalii raia wa Italia kutoa shukrani zao kwa namna askari hao walivyowahudumia, baada ya kukumbana na changamoto ya kiusalama ya jaribio la kutapeliwa.

“Askari  hao wamekua mfano bora wa kuigwa kwa kuitangaza Nchi yetu vizuri Kimataifa hususani kipindi hiki ambacho Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anautangaza utalii kupitia filamu ya The Royal Tour,” ameisitiza Masauni.

Aidha amesema Serikali itandelea kuwathamini na kuwapongeza Askari wote wazalendo na waadilifu wanaotekeleza majukumu yao vizuri popote Nchini.

Pia amekemea vitendo viovu kwa baadhi ya Askari wachache ambao sio waadilifu, ambapo amewataka kuacha tabia hizo kwani zinachafua taswira ya Jeshi la Polisi na nchi kwa ujumla.

Send this to a friend