Askari waliofukuzwa kazi Arusha washitakiwa kwa uhujumu uchumi

0
33

Askari Polisi watatu na raia watano akiwemo mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite jijini Arusha, Lucas Mdeme (46) wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha wakikabiliwa na mashtaka sita ikiwemo uhujumu uchumi.

Mashitaka mengine ni utakatishaji fedha haramu na kupanga njama za kujipatia fedha (ya awali) TZS milioni 10 kati ya TZS milioni 30 walizohitaji kutoka kwa Sammy Mollel.

Askari hao ambao tayari wamefukuzwa kazi kwa tuhuma ya rushwa ni askari mwenye namba G. 5134, DC Heavenlight Mushi aliyekuwa askari kitengo cha intelijensia Mkoa wa Kipolisi Kinondoni jijini Dar es Salaam, H.125 PC, Gasper Paul wa kitengo Cha Intelijensia Makao Makuu Dodoma na H.1021 PC Bryton Murumbe aliyekuwa Askari wa kawaida Mkoani Dodoma.

Mbali na Mdeme, raia wengine waliopandishwa kizimbani ni Joseph Chacha (43) maarufu kwa jina la mkazi wa Ilboru, Leonila Joseph (46), mkazi wa Ilboru, Nelson Lyimo (58) mkazi wa Kijenge Juu na Omary Alphonce (43, mkazi wa Olasiva jijini Arusha.

Katika kesi ya msingi, shitaka la kwanza linawakabili mshitakiwa wa 1, 2 na 3 ambao ni Askari ambao wanadaiwa Disemba 5, 2020 walijihushisha na uhalifu huku wakitambua kuwa wao ni watumishi wa umma na kujipatia rushwa ya awali ya kiasi cha TZS milioni 10 kutoka kwa Sammy Mollel ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Gems & Rock Venture ya jijini Arusha.

Shitaka la pili linawakabili washitakiwa wanne ambaye ni Chacha (maarufu Baba Ngodo) ,mshtakiwa wa tano Joseph, mshitakiwa wa sita Lyimo, mshitakiwa wa saba Mdeme na mshtakiwa wa nane Alphonce (maarufu Matelephone) wote wanashitakiwa kwa kujifanya watumishi wa umma na kuunda mtandao wa kihalifu na kupanga njama za kujipatia fedha taslimu TZS milioni 10 kutoka kwa Mollel.

Shitaka la tatu linawakabili watuhumiwa wote nane ambalo ni la kupanga njama za kuhujumu uchumi kwani Disemba 5 mwaka jana waliweza kujipatia fedha TZS milioni 10 kutoka kwa Mollel.

Mwendesha mashitaka wa serikali amesema shitaka la nne linamkabili Chacha, mshitakiwa wanne, ambaye anatuhumiwa akiwa na nia kufanya uhalifu na udanganyifu na kujitambulisha kuwa yeye ni mtumishi wa umma, Ikulu.

Shitaka la tano linawahusisha washitakiwa wote kwa kufanya udanganyifu na kujipatia fedha kiasi cha TZS milioni 10 za awali kati ya TZS milioni 30 ili wamwachie huru kwa tuhuma za kukwepa kodi na kufanya biashara ya madini ya Tanzanite kwa kutorosha madini nje kinyume cha sheria.

Pia, watuhumiwa wote wamesomewa shitaka la sita la utakatishaji fedha haramu kwamba kwa pamoja Disemba 5 mwaka jana walipatia fedha kwa njia ya udanganyifu TZS milioni 10 kutoka kwa mfanyabiashara Sammy Mollel.

Mara baada ya kusomewa mashitaka hayo Hakimu Ngoka aliwaeleza watuhumiwa wote kuwa hawatakiwi kujibu chochote kwani mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza mashitaka hayo.

Watuhumiwa wamepelekwa rumande hadi Januari 27 mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.

Send this to a friend