Askofu Shoo awaonya wanaotumia mamlaka kuwaumiza wengine

0
72

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dkt. Fredrick Shoo amewatahadhari watu wanaotumia nafasi, nguvu na mamlaka waliyonayo kusababisha maumivu na machungu kwa watu wengine na kuwataka kubadilika.

Dkt. Shoo ambaye pia Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini amesema hayo katika salamu zake za Sikukuu ya Krismasi na kuongeza kwamba ni wajibu wa kila mmoja kuitumia siku hii muhimu kwa Wakristo wote duniani kutafuta amani na furaha kwa wengine na kuepuka kuwasababishia watu huzuni na uchungu.

“Ni kweli yapo mambo yanayoendelea katika jamii na nchi yetu, wapo watu wanaosababisha wenzao wakose amani, wamewasababishia maumivu na uchungu moyoni, maumivu ambayo yamegusa hata familia za hao wenzetu, wamefanya hivyo kwa sababu tu wanayo nguvu, wana nafasi na wana mamlaka,” amesisitiza.

Amewaasa kutumia sikukuu hii kumshukuru Mungu kwenye mengi aliyowapitisha tangu Krismasi iliyopita na waombe Mungu awape neema ya kuumaliza mwaka huu kwa amani na kuuanza mwaka 2022 na ukawe mwaka wa baraka.