ATCL yafafanua hitilafu iliyotokea kwenye injini ndege ikiwa angani
Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) imesema hitilafu iliyotokea katika ndege yake aina ya Airbus A220-300 iliyokuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda jijini Mbeya kwenye moja ya injini zake Februari 24 mwaka huu lilikuwa ni jambo dogo na la kawaida kwenye ndege.
Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Mhandisi Ladslaus Matindi amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni siku chache baada ya kuenea kwa taarifa mbalimbali kuhusu ndege ya shirika hilo kupata hitilafu na kusababisha taharuki kwa abiria.
“Kuna injini moja ilipata joto sana na ikawa na mafuta mengi ndiyo yaliyosababisha moshi ambao uliingia kwenye mifumo ya hewa (AC) na ndiyo sababu moshi huo ukawafikia abiria sio ndege kuungua moto kama ilivyoelezwa,” ameeleza.
Ameongeza kuwa “ule moshi uliendelea kwa takribani dakika tano, na baada ya hizo dakika tano ulikuwa umekwisha na hiyo ilikuwa ni pamoja na kuzima injini moja, na hii ni kawaida ni utaratibu wa kawaida ambapo ndege yetu inaweza ikaenda na injini moja,” amesema.
Matindi amefafanua kuwa kwa kuthamini usalama wa abiria marubani waliamua kurudisha ndege hiyo Dar es Salaam na kutua salama ambapo abiria 104 walikubali kuondoka na shirika hilo, huku abiria 18 wakiomba kubadilishiwa ndege nyingine.