ATCL yakanusha ndege kutelekezwa Malaysia

0
31

Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limekanusha taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa ndege yake aina ya Boeing 787- 8 yenye usajili wa namba 5H-TCJ imepelekwa nchini Malaysia kwa ajili ya matengenezo makubwa kabla ya kufikisha muda wake tangu inunuliwe na kutelekezwa nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na ATCL kupitia Mkurugenzi Mtendaji, Mhandisi Ladislaus Matindi imesema ndege hiyo ipo nchini humo kwa ajili ya matengenezo ya lazima ya injini zake baada ya kufikisha muda wake na sio matengenezo makubwa (Check – C).

“Matengenezo makubwa ya ndege zetu za 787 – 8 (Dreamliner) yanafanyika hapa nchini kwenye Karakana yetu ya KIMAFA iliyopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro kila baada ya miaka mitatu au masaa 12,000 chochote kitakachoanza. Karakana zetu zina wataalam wenye uzoefu wa kufanya matengenezo makubwa ya ndege ya kiwango cha Check – C,” amesema Matindi.

Aidha, amesema tangu ndege hizo ziwasili nchini zimefanyiwa matengenezo makubwa (Check – C) mara moja ambapo kwa ndege ya kwanza iliyowasili nchini mwaka 2018 ilifanyiwa matengenezo hayo mwaka 2021, na ya pili iliyowasili mwaka 2019 ilifanyiwa matengenezo mwaka 2022.

Vilevile amesema tatizo la ndege kukaa muda mrefu kwenye karakana nchini humo linatokana na uhaba wa injini za ziada ambazo zingeweza kutumika wakati injini zake zikifanyiwa matengenezo.

ATCL imebainisha kuwa injini zinapopelekwa kwa ajili ya matengenezo zinalazimika kuzingatia foleni au zamu (slot) kutokana na idadi kubwa ya injini zinazosubiria matengenezo na hivyo kupelekea kuchukua muda mrefu kuhitimisha matengenezo yake.

Imeongeza kuwa kwa sasa matengenezo ya injini za ndege hiyo tayari yanaendelea na inatarajia kurejea nchini mwanzoni mwa mwezi Juni, mwaka huu.

Send this to a friend