Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imezindua ofa ya punguzo kwa wanafunzi wa Kitanzania wanaorejea nchini China kwa ajili ya masomo yao.
Akitoa taarifa hiyo, Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amesema uamuzi wa ATCL umekuja kufuatia malalamiko mengi yaliyotolewa na wanafunzi waliodai kuwa hawawezi kumudu gharama za usafiri.
Tanzania yaijibu Umoja wa Ulaya suala la bomba la mafuta kutoka Uganda
“Wanafunzi wengi walitoa taarifa Ubalozini kwamba hawataweza kumudu gharama za usafiri. Gharama ni kubwa, na kwa kweli zingine ni kubwa zaidi kuliko karo za shule. Tumejadili hili na mamlaka mbalimbali hapa China na nyumbani, kwa hiyo sasa nina furaha kuwajulisha kuwa Air Tanzania imeamua kutoa punguzo la bei kwa wanafunzi,” amesema Balozi Kairuki
Mwanafunzi anayesafiri kwenda China sasa atalazimika kulipa dola 2,100 pekee (takriban TZS milioni 4.8) badala ya dola 3,800 (sawa na TZS milioni 8.8) hadi USD 6,500 (sawa na TZS milioni 15.2).
Balozi Kairuki amesema nauli hiyo mpya pia itashughulikia masuala mengine muhimu kama vile gharama za kukaa karantini nchini kabla ya safari na gharama za vipimo vya UVIKO-19.
Aidha, amesema wanafunzi ambao tayari wameshaanza masomo watatakiwa kuonesha ushahidi kuwa wana visa ya China (visa ya mwanafunzi) na kitambulisho chao cha Chuo Kikuu. Na kwa wanafunzi wapya watahitajika kuonyesha visa ya China na barua au kibali cha kuingia.