Athari za kihisia kwa vijana wanaotegemea AI kama rafiki

Programu ya Akili Mnemba (AI) imekuwa msaada mkubwa katika kutoa majibu kwa masuala mbalimbali na kurahisisha kazi nyingi za kila siku.
Hata hivyo, kwa upande mwingine, imeelezwa kuwa teknolojia hii inaweza kuwa na athari kubwa, hasa pale ambapo watu hususan vijana wanaanza kuipa nafasi kubwa zaidi kuliko mahusiano yao na binadamu wenzao.
Hizi ni athari zinazoweza kujitokeza:
Kupungua kwa uhusiano wa kibinadamu
Vijana wanaweza kushindwa kuzungumza moja kwa moja na watu au kueleza hisia zao kwa wale waliokaribu nao, jambo ambalo linaweza kuwafanya wajitenge na jamii na kupoteza imani kwa binadamu.
Mila na desturi
Mfuatiliaji na Mtathimini wa masuala ya Kijamii na kisaikolojia, John Ambrose ameeleza kuwa kila mtu amekuzwa katika mila na desturi ya eneo fulani, akili mnemba inaweza kutoa ushauri kinyume na mila desturi ya mtu.
“AI haijibu kwa kuangalia tamaduni au desturi zako, yenyewe ni roboti ambayo inaangalia muktadha uliopo. Inafanya kazi katika kiwango cha ulimwengu, maana yake inachuka watu wote inaweka kwenye fungu moja, kwahiyo inakushauri kutoka kwenye fungu, licha ya kuwa tuna fotauti nyingi zinazotokana na mazingira. Unapozungumza na binadamu inaweza kukupa ule uhalisia,” amesema.
Kuweka matarajio yasiyo halisi
AI hujibu kwa njia ya utulivu pasipo kukumu, jambo ambalo linaweza kuwafanya vijana wasitarajie changamoto au hisia halisi kutoka kwa watu wa kweli na kutegemea watu kuwa kama AI.
Kuondoa uwezo wa kujitegemea
Mwanasaikolojia Ambrose anaeleza kuwa akili mnemba inaweza kulemaza akili za watu na kushindwa kujitegemea au kushindwa kukabiliana na hali au changamoto kwenye maisha ya kawaida.
Hatari ya upweke wa kihisia
Ingawa AI inaweza kusikiliza au kujibu kwa njia ya huruma, haiwezi kuelewa kwa undani mateso ya kiakili au kihisia kama binadamu anavyoweza.
“Unapozungumza na mtu kuna kitu cha tofauti, kile cha ubinadamu ambacho tunakiambatanisha kwenye hisia, suala la hisia lina umuhimu zaidi,” ameeleza.
Kupuuza mawazo ya wengine
Vijana wanaotegemea AI wanaweza kupuuza ushauri wa wazazi, marafiki au wataalamu wa afya ya akili, kwa sababu wanajisikia wana mtu wa kuzungumza naye licha ya kuwa ni roboti.
Maudhui yasiyo sahihi
AI haijui kila wakati mipaka ya ushauri salama au wa kisheria, na inaweza kutoa maelezo yasiyo sahihi au yasiyofaa.








