Athari za kuwasha taa za ‘hazard’ kwenye makutano ya barabara na

0
91

Mara kwa mara tumekutana na madereva ambao wakiwa wamesimama kwenye alama za waenda kwa miguu (Zebra Cross) kupisha watu wavuke au wakiwa kwenye makutano ya barabara ya msalaba (cross junction) yasiyoongozwa na taa huwasha taa mbili zenye kuwaka na kuzima maarufu kama ‘hazard’.

Matumizi ya taa hizi yamekuwa yakichanganya sana, na wakati mwingine tumesikia madereva wakilalamikia kulazimishwa na askari kuwasha ‘hazard’ wanaposimama kwenye alama za kuvuka waenda kwa miguu. Lakini swali ni je, sheria inalazimisha kuwasha taa hizo katika mazingira hayo? Na je endapo utawasha, yapi yanaweza kuwa madhara yake?

Kabla ya kujibu swali hili, kwanza tukumbushane kuwa tunaishi kwenye ulimwengu wa kimataifa ulio na mtangamano (integrated world) ambapo barabara za nchi moja hazitumiki na watu wa nchi hiyo tu bali hutumika pia na wageni. Hii ndio sababu alama za msingi za barabarani zinafanana karibu duniani kote.

Alama ya STOP utakayoiona Tanzania ndiyo hiyo hiyo utakutana nayo penginepo ulimwenguni. Tunachotofautiana sana ni alama za ziada (secondary signs). Jambo hili litupe picha ya madhara tunayoweza kupata barabarani ikitokea kuna mchanganyiko wa watu wa mataifa mbalimbali.

Matumizi ya hazard na madhara yake
Taa za hazard hutumika kuashiria dharura aliyonayo dereva anayeziwasha taa hizo. Hivyo kuonesha uhitaji wake wa msaada au kuashiria hatari anayokabiliwa nayo.

Sasa endapo dereva atakuwa barabarani akawasha hazard huku akiwa amesimama au kuegesha gari, moja kwa moja dereva wa nyuma atatafsiri kuwa dereva huyo wa mbele ana dharura, hivyo atakachofanya ni kumpita (overtake).

Na kwa upande wa makutano, endapo dereva anayenyoosha moja kwa moja akiwasha hazard anaweza kusababisha dereva wa nyuma ampite au dereva wa upande mwingine asiyeiona taa ya upande wa pili ya huyu dereva kudhani dereva huyu anataka kupinda kulia au kushoto. Matokeo ya mkanganyiko huu ni ajali. Na baada ya ajali madereva hawa wakiulizwa, kila mmoja atasema nilidhani…..nilidhani….ndio maana nikapinda huku.

Kuondoa mkanganyiko huu na hatari ya kugongana au kugonga, sio vizuri kuwasha hazard kwenye zebra au kwenye makutano ya barabara. Taa za breki zinatosha sana kumuashiria dereva wa nyuma kuwa umesimama.

Sheria ya Usalama Barabarani
Sheria mama ya Usalama Barabarani (THE ROAD TRAFFIC ACT Cap 168) na hata Highways Code ya Tanzania ipo kimya katika jambo hili, kwa maana ya kwamba haioneshi popote kama ni lazima dereva kuwasha hazard. Maana hata katika alama zinazofundishwa za kuonesha uelekeo (direction indicators) hazard haimo. Ishara zilizopo ni ishara za indiketa (Direction indicator signal), ishara za breki (Brake light signals) na ishara za mkono (arm signlas).

Kwa mujibu wa kanuni ya 116 ya Highways Code ya Uingereza, ‘hazard warning lights’ zinatakiwa kutumika pale tu gari likiwa limesimama, halitembei ili kuwapa tahadhari watumiaji wengine wa barabara kwamba gari limesimama linazuia mtiririko mzuri wa magari.

Taa hizi hazitakiwi kutumika (a) Kwa ajili ya kuhalalisha maegesho ya gari yasiyo sahihi (labda kama una tatizo la msingi) au maegesho ya gari yaliyo hatari; (b) Unapoendesha au kuvutwa na gari jingine barabarani isipokuwa tu pale unapokuwa katika barabara kuu na unataka kuwaonya wengine kuwa gari lako linaweza kuwa kipingamizi kwao.

Tumelazimika kurejea kwenye sheria za Uingereza kwa sababu sheria ya Tanzania ya usalama barabarani asili yake ni Uingereza, kwa hiyo kunapotokea jambo fulani halina tafsiri ya moja kwa moja au halina kipengele inabidi kurudi Uingereza zilikoanzia sheria hizo kuona zinaelekeza nini.

Send this to a friend