
Mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina la Evaristo Mwambogolo (28), mkulima na mkazi w Ululu wilayani Mbozi mkoani Songwe amefariki duniani baada ya kuchomwa kisu kifuani na Exavery Mwaweza, chanzo kikiwa ni mabishano ya mpira wa miguu kati ya Simba na Yanga.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi mkoani humo, imesema Mwambogolo alifariki dunia akiwa njiani wakati akikimbizwa Zahanati ya Iyula kwa ajili ya matibabu.
“Uchunguzi wa awali umeonesha chanzo cha tukio hilo ni ushabiki wa mpira wa timu ya Simba na Yanga kati ya marehemu ma mtuhumiwa, ambapo mtuhumiwa alitumia kisu alichokuwa nacho wakati wa ugomvi huo mara baada ya kutenda kosa hilo, alitoroka kusikojulikana, ” imesema taarifa.
Aidha, Jeshi hilo limesema linafanya msako mkali wa kumtafuta mtuhumiwa huyo ili akamatwe na aweze kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuepuka kujichukulia sheria mkononi na kutojihusisha na vitendo vya vurugu vinavyoweza kusababisha madhara makubwa.







