Aweso: Rais Samia ameimarisha kwa kasi huduma ya maji mijini na vijijini

0
56

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Suluhu, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama imeimarika kwa wananchi wa vijijini kutoka wastani wa asilimia 70.1 mwaka 2020 hadi asilimia 77 mwezi Desemba, 2022 huku upande wa maeneo ya mijini kutoka wastani wa asilimia 84 mwaka 2020 hadi wastani wa asilimia 88 mwezi Desemba, 2022.

Ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2023/2024.

Waziri Aweso amebainisha kuwa takwimu zinaonesha mahitaji ya maji nchini kwa sekta mbalimbali mwaka 2022 yalikuwa ni wastani wa mita za ujazo bilioni 62 na yanatarajiwa kuongezeka na kufikia mita za ujazo bilioni 80.2 mwaka 2035.

“Mahitaji hayo yataendelea kuongezeka kutokana na ongezeko la watu, ukuaji wa shughuli za uzalishaji mali katika sekta mbalimbali hususani kilimo cha umwagiliaji, uzalishaji wa umeme, uzalishaji viwandani, utalii, uchimbaji madini, ufugaji, uvuvi na wanyama pori,” amesema

Aidha, amesema katika kipindi cha miaka miwili sekta ya maji imefanikiwa kukamilisha miradi 1,373 ya usambazaji maji na kuanza kutoa huduma kwa wananchi waishio katika vijiji 2,649 ambako kunafikisha jumla ya vijiji 9,737 vyenye huduma ya maji nchini huku akieleza kuwa ubora wa maji katika vyanzo vya maji, mifumo ya usambazaji nchini ukiendelea kukidhi viwango kwa matumizi yaliyokusudiwa.

Send this to a friend