Baada ya siku 226 rumande, Mbowe na wenzake waachiwa huru

0
40

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) amemuachia huru Mwenyekiti wa Chama cha Deemokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe pamoja na wenzake watatu leo Machi 4, 2022.

DPP amewasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, hatua ambayo imepelekea Mbowe na wenzake watatu kuachiliwa huru mara moja.

Serikali iliwasilisha taarifa yake mahakamani hapo ambayo iliomba kuondoa makosa yote ya washitakiwa hao watatu.

“Taarifa hii tunaiwasilisha kwa njia ya maandishi, kwa maombi hayo ya Kifungu cha 91(1) tunaomba kuondoa mashtaka yote dhidi ya washitakiwa wote sababu zote zipo katika Nole Prosequi ambayo tumeiwasilisha” alisema wakili wa serikali mbele ya Jaji Joachim Tiganga ambaye amekuwa akisimamia kesi hiyo.

Kuachiwa kwa Mbowe na wenzake ambao wamesota rumande kwa siku 226 kumefanyika siku ambayo walitakiwa kuanza kutoa utetezi wao baada ya mahakama kuwakuta na kesi ya kujibu.

Washitakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashitaka ya ugaidi na uhujumu uchumi waliyokuwa wanadaiwa kuyapanga maeneo mbalimbali nchini.

Mbowe alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mara ya kwanza Julai 26, 2021 na kusomewa mashtaka mawili na kisha kesi hiyo kuhairishwa hadi Agosti 5, 2021 kusubiri nyaraka ili kesi yake ihamishiwe mahakama kuu.

Wananchi waliokuwa wamejitokeza mahakamani hao walionekana wenye furaha huku wakishangilia baada ya mwanasiasa huyo wa upinzani kufutiwa kesi hiyo.

Machi 2 mwaka huu viongozi wa dini nchini wakiwa Ikulu jijini Dar es Salaam walimuomba Rais Samia Suluhu Hassan kwa nafasi yake kwamba busara itumike kesi hiyo iondolewe.

 

Send this to a friend