Baba akamatwa akitaka kumuuza mtoto ili anunue pikipiki

0
45

Jeshi la Polisi nchini Liberia linamshikilia mwanaume raia wa Sierra Leone mwenye umri wa miaka 29 na kumshitaki kwa tuhuma za kutaka kumuuza mwanae wa kiume mwenye miaka 10.

Baba huyo alitaka kumuuza mwanae ili aweze kununua pikipiki amlipe rafiki yake.

Amewaambia maafisa wa upelelezi kwamba alihitaji $1,000 (TZS milioni 2.3) kwa ajili ya kununua pikipiki amlipe rafiki yake, kwani iliyokuwa nyumbani kwake iliibwa.

Amesema alipewa ushauri kwamba njia pekee ya haraka ya kupata fedha hizo ni kwenda nchini Liberia kutafuta mteja atakayemnunua mwanae kwani ingekuwa rahisi kufanya hivyo kwenye nchi nyingine.

Katika mpango wa kumuuza uliofanyika Desemba, mtoto huyo alitajwa kwenye mazungumzo yao kama kuku, ili kuepusha watu kujua kwamba walikuwa wakifanya biashara ya kumuuza binadamu.

Baada ya polisi kupata taarifa na kumkamata, mtoto huyo amewekwa chini ya uangalizi wa wizara inayohusika na masuala ya jinsia.

Biashara ya kusafirisha binadamu ni moja ya changamoto kubwa zinazokabili nchi za Magharibi mwa Afrika, ambapo watoto huuzwa na kutumikishwa kwa kazi za majumbani huku wakipigwa marufuku kuwasiliana na familia zao.

 

Send this to a friend