Baba aliyeua watoto wake watatu ahukumiwa miaka 150 jela

0
14

Mahakama Kuu ya Bomet nchini Kenya imemhukumu kifungo cha miaka 150 jela mwanaume aitwaye Benard Kipkemoi Kirui mwenye umri wa miaka 40 baada ya kupatikana na hatia ya kuwaua watoto wake watatu katika eneo la Lelaitich, Kaunti ya Bomet.

Kirua amepatikana na hatia ya kuwaua watoto hao ambao ni Amos Kipngetich (12), Vincent Kiprotich (8), na Emanuel Kipronoh (5) wakati mama yao akiwa hayupo nyumbani baada ya ugomvi na mumewe mwaka 2019, ambapo miili ya watoto hao ilikutwa na alama za mikwaruzo shingoni.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Bomet, Justice Julius Kipkosgei Ng’arng’ar, ametoa hukumu hiyo Jumatatu, akisema kila kosa litamfanya mtuhumiwa kutumikia kifungo cha miaka 50 mfululizo.

Jaji Ng’arng’ar alitaja mauaji hayo kuwa ya kikatili na yasiyo ya kibinadamu, na kwamba adhabu hiyo itakuwa mfano kwa wengine wenye nia ya kutenda uhalifu kama huo. Hata hivyo, mtuhumiwa amepewa siku 14 za kukata rufaa.

Taarifa zinaeleza kuwa baada ya kuwaua wanawe watatu mwanaume huyo alijaribu kujitoa uhai kwa kujinyonga, lakini kamba ilikatika.

 

Send this to a friend