Baba amnyonga mwanaye na kumtupa kisimani akidai si damu yake

0
63

Mwanaume aliyejulikana kwa jina Kisumo Emmanuel (38) mkazi wa Sayaka wilayani Magu mkoani Mwanza amemuua mtoto wake Lukonya Kisumo (3) kwa kumnyonga shingo kwa madai kuwa mtoto huyo si wake hivyo amezaliwa nje ya ndoa.

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema baada ya kutekeleza tukio hilo lililofanyika Julai 28, 2024, baba huyo aliamua kujinyonga kwa kutumia kipande cha shuka na kupoteza maisha.

“Baada ya baba huyo kufanya ukatili kwa mwanaye, aliamua kuutupa mwili wa mtoto wake kwenye kisima cha maji kilichochimbwa kwenye shamba lake la mpunga. Baada ya kutekeleza ukatili huo, baba huyo naye aliamua kujinyonga kwa kipande cha shuka alichokifunga kwenye mti umbali wa kilomita 1 kutoka nyumbani kwake, “ ameeleza.

Ameongeza kuwa “wakati polisi wanamtafuta mtuhumiwa walimpata akiwa ameshafariki dunia, huku mwili wake ukiwa umening’inia kwenye mti ndani ya shamba la jirani yake, umbali mfupi kutoka alipokuwa anaishi.”

Jeshi la Polisi limesema uchunguzi wa miili umeanyika na tayari imekabidhiwa kwa wapendwa wao kwa ajili ya maziko.

Send this to a friend