Baba ampiga risasi binti yake kwa kuchukizwa na maudhui aliyokuwa akichapisha Tiktok

0
2

Mwanaume mmoja aitwaye Anwar ul-Haq, aliyekuwa ameirejesha familia yake Pakistan baada ya kuishi Marekani kwa miaka 25, amekiri kumuua binti yake wa miaka 15 kwa kumpiga risasi kutokana na kutoridhishwa na maudhui aliyokuwa akichapisha kwenye mtandao wa TikTok.

Mauaji hayo yalitokea Jumanne katika mji wa Quetta, Kusini magharibi mwa nchi hiyo, ambapo polisi wamesema mshukiwa awali alidai kuwa watu wasiojulikana walimpiga risasi binti yake mzaliwa wa Marekani kabla ya kukiri kuwa yeye ndiye aliyefanya kitendo hicho.

“Uchunguzi wetu hadi sasa umebaini kuwa familia ilikuwa na pingamizi kuhusu mavazi yake, mtindo wa maisha, na mikusanyiko yake ya kijamii,” amesema mpelelezi wa polisi, Zohaib Mohsin.

Ameongeza kuwa Haq alimwambia kuwa binti yake alianza kuunda maudhui yasiyofaa kwenye mtandao wa TikTok alipokuwa akiishi Marekani na aliendelea kuchapisha video hizo aliporejea Pakistan licha ya kumzuia kufanya hivyo.

Aidha, polisi wanamshikilia shemeji wa mshukiwa kwa kushirikiana na mwanaume huyo kutekeleza mauaji hayo.

Kwa mujibu wa Tume Huru ya Haki za Binadamu ya Pakistan, zaidi ya watu 1,000 wengi wao wakiwa wanawake huuawa kila mwaka kwa kile kinachoitwa mauaji ya heshima. Mauaji hayo yanafanywa na ndugu na jamaa wanaosema wanatetea heshima ya familia zao.