
Hali ya majonzi imetanda katika eneo la Tach Asis, Konoin, Kaunti ya Bomet nchini Kenya, baada ya mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 35 kuwaua watoto wake wawili wenye umri wa miaka miwili na miaka saba kwa kuwakata vichwa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Bomet, Edward Imbwaga, mtuhumiwa anayeitwa Geoffrey Kipkemoi, anadaiwa kutumia kisu cha jikoni kutekeleza tukio hilo la kikatili. Miili ya watoto hao imepatikana ikiwa imehifadhiwa jikoni.
Taarifa ya polisi imeeleza kuwa mke wa mtuhumiwa hakuwepo nyumbani wakati tukio hilo lilipotokea na aliporudi, aligundua tukio hilo baada ya kufuata alama za damu zilizoelekea jikoni, na ndipo alipotoa taarifa polisi.
Maafisa wa usalama walifika eneo la tukio, wakachukua ushahidi na silaha inayodaiwa kutumika. Miili ya watoto hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Kapkatet kwa uchunguzi wa kitabibu, huku mtuhumiwa akiwa chini ya ulinzi wa polisi wakati uchunguzi ukiendelea.