Baba na binti yake washitakiwa kwa kupanga kuua familia kwa sababu ya mali

0
49

Mzee mwenye umri wa miaka sabini na mbili, Antony Muya ameshtakiwa kwa kupanga kumuua mke wake wa zamani na watoto wake wanne kutokana na mgogoro wa umiliki wa kipande cha ardhi nchini Kenya.

Katika kesi hiyo, mzee huyo ambaye ni mkulima akishirikiana na binti yake na mkwe wake waishio Marekani, waliwaajiri wauaji wawili na kukubaliana malipo ya shilingi milioni 2 za Kenya [TZS milioni 42.2] ili kuwaondoa mke wake, watoto wake watatu wa kiume na binti yake.

Hata hivyo, kama bahati ilivyokuwa, wauaji hao baada ya kupokea shilingi milioni 1.7 [TZS milioni 35.9] walivujisha mpango huo kwa wahasiriwa na kuwafahamisha kuhusu njama hiyo kabla ya polisi kuingilia kati na kumkamata mtuhumiwa.

Kulingana na hati za mahakama, mpango huo ulianza Machi 01, wakati Muya na bintiye walipodaiwa kukutana na wauaji hao wawili katika hoteli moja mjini Nakuru, ambapo baba na bintiye walitaka watano hao wauawe kwa kukataa kuondoka katika ardhi hiyo.

Mmoja wa wauaji hao, Paul Waithaka ameeleza kwa kiapo kuwa Muya na binti yake walitaka kuwateka nyara mke wa zamani wa Muya pamoja na watoto wake watatu wa kiume na binti yao, kisha kuwalazimisha kuhamisha umiliki wa ardhi kwa majina yao kabla ya kuwaua.

Hata hivyo, mahakama pia imeagiza kukamatwa kwa washirika wengine wawili ambao wanaishi Marekani, wakidaiwa kuwa walifadhili mpango huo wa mauaji.

Send this to a friend