Baba, Paroko wakamatwa wakiwa na viungo vinavyodhaniwa ni vya mtoto albino aliyeuawa Kagera

0
57

Kufuatia mauaji ya kikatili yaliyofanywa kwa mtoto Asimwe Novart (2) mwenye ulemavu wa ngozi aliyeporwa na watu wasiojulikana katika Kijiji cha Bulamulaa wilaya ya Muleba mkoani Kagera na baadaye kupatikana akiwa amekatwa baadhi ya viungo vyake, Jeshi la Polisi mkoani Kagera limewakamata watu tisa akiwemo baba mzazi wa marehemu wakiwa na viungo vinavyodhaniwa ni vya mtoto huyo.

Katika taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema kwa kushirikiana na raia wema walianza msako mkali kuanzia Mei 31, mwaka huu hadi usiku wa kuamkia Juni 19, mwaka huu ambapo watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa wamehifadhi viungo hivyo katika vifungashio vya plastiki wakitafuta mteja.

“Watuhumiwa waliokamatwa ambao walieleza jinsi walivyoshiriki katika tukio hili ni pamoja na baba mzazi wa mtoto huyo aitwaye Novart Venant, Desideli Evarist ambaye ni mganga wa jadi mkazi wa Nyakahama, Elipidius Rwegoshora, Paroko msaidizi wa Parokia ya Bugandika ambaye anadaiwa kumfuata na kumshawishi baba mzazi wa mtoto ili wafanye biashara ya viungo vya binadamu. Pia anatuhumiwa kuwa ndiye aliyemtafuta mganga wa jadi na kulipia gharama zote za uganga,” imesema.

Watuhumiwa wengine ni Dastan Kaiza, mkazi wa Bushagara, Faswiru Athuman, mkazi wa Nyakahama, Gozibert Aikadi, mkazi wa Nyakahama Kamachumu, Rwenyagira Burkadi, mkazi wa Nyakahama Kamachumu, Ramadhani Selestine, mkazi wa Kamachumu na Nurduni Hamada, mkazi wa Kamachumu.

Hata hivyo Jeshi la Polisi limetoa onyo kali kwa watu wanaoendekeza imani za kishirikina ikiwemo kupiga ramli chonganishi wakiaminisha kwamba wanaweza kupata utajiri kwa njia za kishirikina kuacha mara moja tabia hizo

Send this to a friend