Baba mzazi wa Waziri wa Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson amesema yupo kwenye mchakato wa kuomba hati ya kusafiria (passport) ya Ufaransa ili kuendeleza ukaribu wake na Umoja wa Ulaya (EU) baada Uingereza kujitoa.
Stanley Johnson amesema kuwa anataka kuwa raia wa Ufaransa kutokana na kuwa na historia ya kifamilia na taifa hilo.
“Kama nakumbuka vizuri, mimi ni Mfaransa. Mama yangu alizaliwa Ufaransa, mama yake alikuwa Mfaransa kabisa, kama ilivyokuwa kwa babu yake. Hivyo kwangu ni kung’ang’ania kile ambacho tayari ninacho, na hilo linanifanya niwe na furaha,” amesema Jonhnson.
Katika kura za maoni za mwaka 2016 kuamua endapo Uingereza ijitoe au ibaki ndani ya EU, Johnson amesema kuwa alipiga kura Taifa hilo libaki. Hata hivyo wanaotaka kujitoa walishinda huku mwanae (Boris) akiwa mpigia debe mkuu wa kujitoa akiamini Taifa hilo litaendelea zaidi likiwa nje ya EU.
Jumatano mara baada ya bunge kuidhinisha makubaliano ya kibiashara kati ya Uingereza na EU, Boris alizungumza mithili ya msuluhishi akisema huo sio mwisho wa nchi hiyo kama Taifa la Ulaya.
Uingereza itajitoa rasmi ndani ya Umoja wa Ulaya leo (Disemba 31, 2020) usiku baada ya kuwa ndani ya umoja huo kuanzia 1973.