BAKWATA yaitaka Serikali kutowafumbia macho waliochochea vurugu Oktoba 29

0
84

Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Kiislamu zimeitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini watu wote waliokuwa vinara kuchochea vijana kuvunja amani wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025 na kupelekea maisha ya watu kupotea.

Viongozi hao wamesema tukio hilo limeacha majonzi makubwa kutokana na vifo vya watu wasio na hatia, ulemavu wa kudumu, na uharibifu wa mali na miundombinu ya umma na binafsi.

“Sisi kwa umoja wetu tunalaani vitendo hivvyo vya kihalifu ambavyo udhibiti wake umepelekea vifo vya watu wasio na hatia. Sisi kwa umoja wetu tumeumia sana kwa haya yaliyotokea, hasa maisha ya watu yaliyopotea kutokana na vitendo hivi vya kihalifu,” imesema BAKWATA na taasisi hizo.

Viongozi hao wameeleza kuwa kabla ya Uchaguzi Mkuu, viongozi hao walifanya jitihada kubwa na kutumia muda mwingi kuwaasa waumini kutunza amani na kujiepusha na maneno ambayo yatachochea uvunjifu wa amani, huku wakisisitiza kuwa mahali pasipo na amani haki haiwezi kupatikana.

Aidha, BAKWATA imeiomba serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma na kuwafariji wale wote waliokumbwa na maafa hayo pasipo kuhusika kwa namna yoyote, na kuisihi serikali kuzingatia suluhu na maridhiano kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi, likisisitiza kuwa suluhu na maridhiano yasitumike kama zawadi kwa watu waliohusika na kutekeleza uhalifu uliopelekea maafa hayo.

Send this to a friend