Balozi Dkt. Nchimbi: Dhamira ya Rais Samia ni kuhakikisha nchi inaongozwa kwa kuzingatia misingi ya demokrasia.

0
63

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema dhamira ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha nchi inaongozwa kwa kuzingatia misingi ya demokrasia na utawala bora, hivyo dhamira hiyo haipaswi kutiliwa shaka.

Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle, kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam, ambapo wamejadiliana kuhusu ushirikiano na uhusiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.

Balozi Nchimbi amesema katika utekelezaji wa dhana ya utawala bora, chini ya uongozi wa Rais Samia, Tanzania imeendelea kushuhudia kuwapo kwa uhuru wa mihimili mitatu ya dola, ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama.

Ameongeza kuwa, mihimili hiyo ya dola imeendelea kutimiza wajibu wake kwa kufanya kazi vizuri na hivyo kuaminiwa na wananachi, na kusisitiza kuwa CCM chini ya Rais Samia, itahakikisha dhamira hiyo pia inaendelezwa kwa vitendo.