Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini aelezea hali za Watanzania kutokana na vurugu nchini humo

0
40

Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Richard Lupembe amesema bado mpaka leo Jumanne Septemba 3, 2019 saa 5 asubuhi hakuna Mtanzania aliyeuawa katika vurugu zinazoendelea nchini humo zinazowalenga zaidi wageni.

Vurugu hizo zinazojirudia mara kwa mara ziliibuka jana Jumatatu wakati vikosi mbalimbali vya uokoaji vikizima moto katika jengo moja mjini Jeppestown na kusababisha mauaji ya watu watatu huku watu kadhaa wakiripotiwa kuuawa na kupata majeraha.

Watu waliokuwa kwenye makundi walivamia maeneo yenye shughuli za biashara na kuchoma moto maduka pamoja na kupora.

Akizungumza na gazeti la Mwananchi kwa simu jana Jumanne, Balozi Lupembe amesema hajapokea taarifa ya Mtanzania kuuawa wala kujeruhiwa katika vurugu hizo.

“Kuna karibu siku mbili tatu, lakini hatujapata taarifa kutoka kwa Watanzania na watu wengine katika maeneo hayo kama kuna Watanzania wamefariki,” amesema Balozi Lupembe.

“Mnaona kuna watu wanachomwa moto, sasa bahati mbaya watu wana ‘jump’ ku post (wanakimbilia kurusha) kwamba kuna Watanzania wameuawa, lakini sisi kama ubalozi kwa kutumia vyanzo vyetu hatujapata taarifa kwamba kuna Mtanzania ameuawa,” amesema

Amesema wanaendelea kufuatilia, wakipata Mtanzania yoyote aliyefariki watafanya utaratibu wa kurudisha mwili wake. Hata hivyo, amesema wiki iliyopita kuna tukio la maduka ya Watanzania kuchomwa moto lakini wao wenyewe walitoka salama.

Akifafanua zaidi, Balozi Lupembe amesema vurugu hizo zinatokea kwenye maeneo ya hali ya chini kiuchumi ambako hakuna ulinzi wa uhakika.

“Lazima muelewe kwamba, Afrika Kusini ina matatizo yake, hizo sehemu zinazotokea vurugu ni sehemu za watu wa chini, nikupe mfano kama Manzese (Dar es Salaam). Ni sehemu za watu wa chini, wahamiaji labda na Watanzania wanaokuja kutafuta maisha, ni jumuiya watu wa chini,” amesema.

“Maeneo yale ya uwekezaji kama viwanda kama Sandton hayaguswi hata kidogo. Nikikupa mfano wa haraka ni kama Mazese au Kigogo kule tunaona maisha ya chini ndiko yanakotokea huko. Wao wanalenga maduka kama vile ya chakula na vitu. Kabla ya kuchoma wanachukua mali ndipo wanachoma,” amesema

Ametaja baadhi ya wageni walioathiriwa na uchomaji wa maduka hayo ni pamoja na Wanigeria, Somalia na Ethiopia.

“Hali ya usalama kwenye hizo sehemu za watu wa chini siyo nzuri na Polisi wanajaribu kudhibiti hali lakini inashindikana kwa sababu hao jamaa wanashtukiza, hawatangazi. Kwa mfano kama leo walitangaza kutakuwa na vurugu kubwa, lakini haijatokea mpaka sasa hivi. Jana tulitegemea vurugu itokee asubuhi, lakini tukakaa mpaka mchana ndipo ikatokea,” amesema Balozi Lupembe.

Akifafanua kuhusu chanzo cha vurugu za hivi karibuni, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Afrika Kusini, Mavela Masondo amesema, “Wakati bado tunafanya uchunguzi na huduma za dharura, watu waliokuwepo karibu walianza kutumia fursa ya hali iliyopo na kupora kwenye maduka.”

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), ghasia hizo zilianzia katika eneo la Jeppestown, lililopo katika wilaya ya kati yenye shughuli za biashara na kusambaa hadi kwenye maeneo mengine ya Denver, Malvern, Turffontein, Tembisa na baadhi ya vitongoni ya mji wa Johannesburg.

Video zilizosambaa katika mitandao mbalimbali zinaonyesha magari yakiwa yamechomwa moto. Polisi wamefyatua mabomu ya machozi na risasi za plastiki kujaribu kusitisha uporaji, huku watu 41 wakikamatwa wakiwa na mali walizopora.

Luteni Generali Alias Mawela ambaye ni kamanda wa polisi wa jimbo amesema polisi wamewakamata watu katika ghasia hizo ambazo hata hivyo haijulikani mwanzilishi wake.

HT: Mwananchi

Send this to a friend