Bandari ya Dar es Salaam yaanza kupokea meli kubwa za mizigo baada ya maboresho

0
33

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesema imeendelea kupokea meli kubwa za mizigo katika bandari ya Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya mafanikio baada ya uwekezaji mkubwa na maboresho mbalimbali ya kiutendaji na utoaji huduma yaliyofanyika katika bandari hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa kwenye hafla fupi ya kuipokea meli kubwa ya mizigo ya EverGreen Line Group ikitokea nchini China yenye uwezo wa kusafirisha zaidi ya makontena 4000, Meneja wa Zimamoto na Usalama wa mamlaka hiyo, Mussa Biboze amesema uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika Bandari hiyo, umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi wa kiutendaji, hivyo kuvutia kampuni nyingi za nje kuleta meli zao kwenye bandari hiyo.

Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni ya EverGreen Line group Tawi la Tanzania, Mohamed Lotfy amesema awali walikuwa wanaleta mizigo kupitia meli ndogo, lakini hivi sasa wameamua kuja na meli kubwa kutokana na uwekezaji uliofanywa katika bandari hiyo.

Meneja Kitengo cha Biashara na Mahusiano wa Tanzania East Africa Gateway Terminal Ltd. Donald Talawa amesema ni mafanikio makubwa kupata meli kama hiyo yenye uwezo wa kuchukua makontena mengi.