Bangi yawaponza polisi na afisa usalama wilayani Arumeru

0
13

Rais wa Tanzania Dkt Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi kwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Arumeru na Afisa Usalama wa Wilaya hiyo mkoani Arusha kwa kushindwa kutumiza majukumu yao.

Rais ametoa agizo hilo mapema leo wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua karibu na kueleza kuwa haiwezekani maafisa hao wakashindwa kubaini uwepo wa bangi katika eneo lao, hadi zilipokamatwa na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, James Kaji.

Katika operesheni iliyofanyika hivi karibuni mkoani humo zaidi ya tani mbili za dawa za kulevya aina ya bangi zilikamatwa na kuchomwa moto na mamlaka hiyo.

Akizungumza Rais Magufuli amesema uzembe wa wasaidizi wake kushindwa kubaini uwepo wa dawa hizo unafanya Taifa kutengeneza watu wanaotumia dawa za kulevya.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amempandisha cheo James Kaji kuwa kamishna jenerali wa mamlaka hiyo ambapo awali alikuwa akikaimu nafasi hiyo.

Akitangaza uamuzi huo wa kumthibitisha Kaji pamoja na kumuapisha, Rais Magufuli amesema anachotaka kuona ni matokeo ya kazi wanazofanya wasaidizi wake.

Send this to a friend