Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameagiza kuondolewa kwa Mhandisi Mshauri, LEA Associaties anayesimamia ujenzi wa barabara ya Kitai – Lituhi sehemu ya Amani Makoro-Ruanda (km 35) kwa kiwango cha lami na kuutaka Wakala wa Barabara (TANROADS) kuendelea kusimamia ujenzi huo ili uweze kukamilika.
Hatua hiyo imefuata baada ya kushindwa kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ambayo ilipaswa kukamilika Desemba 2023, lakini mpaka sasa maendeleo ya mradi huo ni asilimia 25 ikilinganishwa na asilimia 100.
Bashungwa ametoa agizo hilo leo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wakati akikagua ujenzi wa barabara hiyo ambapo pia ameagiza mkandarasi anayejenga barabara hiyo, China Railway Seventh Group kutopewa miradi mipya mpaka hapo atakapokamilisha miradi aliyopewa katika mkoa wa Mara, Katavi ambayo nayo inaonekana kusuasua.
“Nimuagize Katibu Mkuu kuangalia hatua za kimkataba mnazotakiwa kumchukulia haraka mhandisi mshauri kwasababu ameshindwa kumsimamia mkandarasi kukamilisha mradi huu kwa wakati,”amesisitiza.
Amesema Rais Samia Suluhu tayari alishatoa TZS bilioni 6.9 ambayo imekamilisha kipande cha kwanza cha kilometa 5 kutoka Kitai hadi Amani Makoro na TZS bilioni 60 kwa ajili ya muendelezo wa barabara hiyo sehemu ya Amani Makoro – Ruanda.