Barabara ya mwendokasi yajengwa chini ya kiwango, Mbarawa atoa maagizo

0
65

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amemtaka mkandarasi anayejenga barabara ya mwendokasi kutoka Kariakoo hadi Mbagala kurudia kipande cha kilometa mbili ndani ya miezi miwili kutokana na kujengwa chini ya kiwango.

Prof. Mbarawa ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya ukaguzi wa barabara, zikiwemo barabara za Mbagala na Kimara hadi Kibaha mkoani Pwani na kuagiza wakandaraasi wanaofanya makosa wanyimwe tenda za serikali ili iwe funzo.

“Ujenzi huu upo chini ya kiwango, naomba mkandarasi ufumue kipande chote cha kilometa mbili na kujenga upya. Mtu wa kawaida anaweza kuona ni kitu kidogo lakini baada ya magari kupita tatizo litazidi kuwa kubwa. Kama tusingeona tungekuwa tumeliwa,” amesema Mbarawa.

Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila amesema barabara hizo zimeanza kuharibika kabla ya kutumika kwa sababu mchanga uliotumika kujenga ulikuwa na udogo wa mfinyanzi.

Barabara hiyo inajengwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza iligharimu shilingi bilioni 217 na awamu ya pili bilioni 45, na mradi mzima unatarajiwa kukamilika Machi 2023.