Barabara za Kampala kufungwa kupisha sherehe za ‘birthday’ ya Rais Museveni

0
45

Barabara kadhaa zinatarajiwa kufungwa katika Mji mkuu wa Uganda, Kampala, siku ya Ijumaa Septemba 08, 2023 kwa ajili ya sherehe za kuadhimisha miaka 79 ya kuzaliwa kwa Rais Yoweri Museveni.

Kamanda wa Usalama Barabarani Jiji la Kampala, Godwin Arinaitwe amesema watafunga barabara ili kupisha sherehe zinazotarajiwa kuhudhuriwa na takribani wageni 100,000 ambazo zitafanyika katika Uwanja wa Uhuru.

“Tunatarajia karibu wageni 100,000 ambao watakuja kutoka sehemu tofauti za nchi. Tunatoa wito kwa umma na wageni kuwa waangalifu, lakini pia kufuata miongozo ya trafiki ili kuepusha usumbufu,” ameagiza kamanda Arinaitwe.

Licha ya kuwa tarehe rasmi ya kuzaliwa kwa Rais Museveni ni Septemba 15, sherehe hizo zimepangwa kufanyika leo zikiandaliwa na vijana ambao wanaongozwa na Mratibu wa Kitaifa katika Ofisi ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha National Resistance Movement (Chama Tawala), Hadijah Namyalo.

Send this to a friend