Barabara za mwendokasi kufungwa vizuizi vya umeme kuzuia magari binfasi

0
53

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka mkoani Dar es Salaam (DART) unatarajia kuweka vizuizi kwenye vituo vyake vya mabasi ili kuzuia magari na pikipiki za watu binafsi kupita katika njia ya mabasi hayo.

Vizuizi hivyo vitafungwa vifaa maalum (sensors) vitakavyanya vizuizi hivyo kufunguka pale tu mabasi yanapokaribia lakini havitafunguka pindi magari na pikipiki binafsi yanapopita njia hizo.

Akizungumza Kaimu Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa DART, Ng’wanashingi Gagaga amesema viuizi hivyo vitasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa ajali za mara kwa mara kati ya mabasi yaendayo haraka, magari binafsi na pikipiki zinazopita katika njia hizo.

Gagaga amesema tayari wamesaini mkataba na mkandarasi ili kuanza ujenzi wa vizuizi ambavyo vitaanza kutumika katika njia ya Kimara- Kivukoni.

“Muda wa mkataba ni wiki 32 kwa hiyo tunategemea vizuizi vitakuwa vimewekwa mwishoni mwa mwaka huu na tutaondokana na kero za kuvutana na wamiliki wa magari binafsi kwa sababu hawataweza tena kupita kwenye njia za mabasi yaendayo haraka,” amesema.

Ameongeza kuwa “hakuna anayeruhusiwa kupita kwenye hizi barabara isipokuwa magari ya mwendokasi, watu wamekuwa wakipita kwenye hizi barabara kwa ukaidi na tumekuwa tukijaribu kupambana nao, tumefanya juhudi kubwa lakini bado wamekuwa wakitumia hizi barabara.”

Send this to a friend