Baraza la Ulamaa limesema ndoa ya Dkt. Mwaka na mkewe haijavunjika

0
82

Baraza la Ulamaa la Kiislamu limesema ndoa ya Juma Mwaka Juma maarufu Dkt. Mwaka na mkewe Queenie Oscar Masanja haijavunjika, hivyo malalamiko ya kesi hiyo yaendelee katika ofisi ya Qadhi.

Uamuzi huo umefikiwa leo Januari 27, 2023 baada ya baraza hilo kukutana kwa dharura kwa ajili ya masuala mbalimbali ikiwemo suala hilo linalowahusisha Dkt. Mwaka na mkewe.

Aidha, baraza limesema muhimili wa mahakama ya Qadhi ni muhimili muhimu na unaojitegemea, hivyo si sahihi maamuzi yake kuingiliwa na mamlaka za BAKWATA Wilaya au Mkoa, na pale suala litakaposhindikana katika mahakama ya chini, suala hilo litapanda katika ngazi ya juu ndani ya muhimili huo huo na si vinginevyo.

“Baraza la Ulamaa linapenda kusisitiza kuwa utaratibu uliowekwa wa mgawanyo wa madaraka kuanzia katika ngazi zote ni muhimu utaratibu huu ukafuatwa na kudumishwa kwa ajili ya kuchunga dhana nzuri ya utawala bora ndani ya baraza,” imesema taarifa ya baraza.

Hata hivyo baraza hilo limesema linafuatilia kwa ukaribu juu ya namna shauri hilo na mengine yanayoendelea kwa ajili ya kuchunga nidhamu katika baraza, vile vile limewafahamisha Waislamu wote kuwa wanapoona kuna upindishwaji wa mambo wasisite kufuata utaratibu wa kuwasiliana na baraza.