Barrick Tanzania yashinda tuzo tano za usalama mahali pa kazi
Barrick Tanzania imeshinda tuzo tano katika hafla ya utoaji wa tuzo za Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ya 2024 iliyofanyika jijini Arusha ambapo Mgodi wa Dhahabu wa Barrick Bulyanhulu umeshinda tuzo kubwa ya mshindi wa juu wa jumla katika Tuzo ya Afya na Usalama (OHS) 2024.
Maonyesho ya OSHA mwaka huu yamefanyika jijini humo mgeni rasmi akiwa ni Naibu Waziri wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Patrobas Katambi aliyemwakilisha Waziri Deogratius Ndejembi.
Mbali na ushindi huo mkubwa, Bulyanhulu pia ilinyakua tuzo za utawala bora ofisini, usaidizi wa kiofisi na shughuli za ukuzaji biashara, na mshindi bora wa ubunifu kwenye maonyesho ya OSHA ya mwaka huu kwenye sekta ya madini huku Barrick North Mara ikishinda tuzo ya juu katika kuwajali zaidi Wafanyakazi wenye Mahitaji Maalum.
Barrick Tanzania imeshinda tuzo za 2024 kutokana na mafanikio ya 2023 ya kampuni ambapo ilishinda tuzo ya jumla ikiwemo tuzo za uandaaji Ripoti Bora ya Tathmini ya Hatari katika uchimbaji madini na mshindi Bora wa Tuzo ya Usalama na Afya (OHS) katika sekta ya madini.
Tuzo nyingine ilizoshinda zilikuwa ni Kujali zaidi Wafanyakazi wenye Mahitaji Maalum na utekelezaji sera bora ya Usalama mahali pa Kazi (OHS), mshindi wa pili kwa washindi wa jumla wa sekta ya Madini, utekelezaji Mpango Kazi Bora wa Usalama na Afya mahali pa kazi.