Barua ya Profesa Shivji kwa Rais Samia

0
44

Kwa heshima na taadhima pokea barua yangu nikikutumia kwa nia njema na katika kutekeleza wajibu wangu kama mwananchi na mwanazuoni kwa mujibu wa Ibara 26 ya Katiba “kuhakikisha hifadhi ya Katiba na sheria za nchi.”

Awali ya yote nakutakia maisha marefu yenye afya njema na furaha tele ili uendelea kutuongoza kwa busara na hekima na kwa kulinda Katiba yetu bila hofu au upendeleo.

Katika sakata la Loliondo na Ngorongoro nimesikia mara kwa mara Waheshemiwa Mawaziri husika wakitamka Bungeni kwamba ardhi yote nchini ni mali ya umma na hakuna mwenye ardhi. Kwa heshima, kwa maoni yangu, tafsiri hiyo ya sheria sio sahihi.

Ni kweli kwamba Sheria ya Ardhi inasema ardhi yote nchini ni ‘public lands’ yaani ardhi ya kiumma na imewekwa mkononi mwa Rais kama mdhamini kwa niaba ya wananchi. Kifungu 4, kifungu kidogo 1, cha Sheria ya Ardhi 1999 (sura 113) kina tamka kwamba ardhi yote nchini Tanzania itaendelea kuwa ardhi ya kiumma na itaendelea kuwa mkononi mwa Rais kama mdhamini kwa niaba ya wananchi wa Tanzania.

Kifungu hiki kinahitaji ufafanuzi. Kwa nini sheria inatumia neno ‘itaendelea’? Kwa sababu tangia mwaka 1923, sheria ya ardhi ya kikoloni ili tamka kwamba ardhi yote nchini ni ardhi ya kiumma na ikawekwa mkononi mwa Gavana. Mfumo huo haukubadilika baada ya Uhuru isipokuwa tu badala ya neno ‘Gavana’ ikawekwa neno ‘Rais’. Mfumo huu umeendelezwa na Sheria ya Ardhi ya 1999 ambayo ni sheria mama kuhusu mfumo wa umilikaji ardhi (land tenure system) Tanzania.

Napenda ni sistize jambo moja. Kifungu hiki hakisemi, wala hakimaanisha, kwamba ardhi ni mali ya umma. Kinainisha tu ardhi kama ardhi ya kiumma na sio tamko la umilikaji ardhi. Kuna tofauti ya msingi kati ya kuainisha ardhi na kumilikisha ardhi. Neno ‘mali’ halipo kabisa katika kifungu hiki. Kwa hivyo, ardhi sio mali ya umma wala ya Rais wala ya Serikali. Kama hivyo ilivyo, basi ardhi ni mali ya nani?

Kifungu cha 4, kifungu kidogo cha 3, kinasema kwamba wote waliokuwa wana kaalia ardhi kabla ya Sheria ya 1999 kwa hati rasmi au kwa mujibu wa mila na desturi wataendelea kukaalia ardhi hiyo. Kifungu kidogo hiki kinaendelea kusisitiza kwamba ukaaji wa ardhi chini ya hati rasmi au kwa mujibu wa mila na desturi itahesabiwa kama mali (‘property’). Katika kifungu hiki mara ya kwanza sheria inatumia neno mali, kwa Kiingereza, property. Kifungu hiki kinaendelea kusisitiza kwamba pamoja na ukaaji kuwa mali, pia matumizi ya ardhi kama malisho ya mifugo kwa mujibu wa sheria za mila na desturi inahesabiwa kuwa mali. Moja kwa moja, sheria imeweka wazi kabisa kwamba matumizi ya ardhi na wafugaji kwa malisho ya mifugo yao inahesibiwa kama mali, yaani property.

Sasa ardhi ni mali ya nani? Ardhi ni mali ya wenye hati rasmi au jamii au kaaya au watu binafsi wanaokaalia ardhi kwa mujibu wa mila na desturi, pamoja na wafugaji ambao hutumia ardhi yao kama malisho. Hao ndio wenye ardhi, sio umma wala Rais wala serikali. Kwa hivyo, sio sahihi kabisa kusema kwamba ardhi ya Tanzania haina wenyewe.

Tafsiri ya sheria niliyotoa hapo juu iliwekwa wazi na Mahakama ya juu kabisa nchini, Mahakama ya Rufaa katika kesi ya Mwanasheria Mkuu dhidi ya Lohay Akonaay na Joseph Lohay iliyoamuliwa mnamo mwaka wa 1994 na kuchapishwa rasmi katika Ripoti za Kesi, Tanzania (Tanzania Law Reports) [1995] T.L.R. 80). Ninanukuu kipengele muhimu cha uamuzi huo:

“Haki za ardhi chini ya mila na desturi, ingawa kwa uhalisia wake ni haki ya kukaa na kutumia ardhi, bado ni mali [property] ambayo inalindwa na ibara 24 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na utwaaji wa haki za mila bila fidia ya haki inazuiliwa na Katiba.” (uk. 81).

Kama kweli hii ndio sheria ya nchi kwa nini upotoshaji na Waheshemiwa Mawaziri umeendelea bila kupingwa au kusahihishwa? Kwa nini Waheshemiwa Mawaziri wanapotamka kwamba ardhi ya Tanzania ni mali ya umma hawabanwi, (kama wanaobanwa waheshimiwa wabunge wengine), kunukuu kifungu cha sheria kinachosema ardhi ni mali ya umma?

Kwa kadri ya uelewa wangu, mwenye dhamana na wajibu wa kutoa tafsiri ya sheria Bungeni na kushauri wabunge (bila kujali vyama vyao) na Bunge juu ya sheria ni Mwanasheria Mkuu. Kama tunajuwa, hatimaye kauli ya mwisho juu ya tafsiri ya sheria ni Mahakama lakini anyetakiwa kutoa tafsiri ya sheria Bungeni pale ambapo kuna ubishi ni Mwanasheria Mkuu, sio Mheshemiwa Spika wala mbunge mwingine yeyote hata kama yeye ni mwanasheria.

Kwa kuwa tafsiri ya sheria iliyotolewa na Mahakama ya Rufaa katika kesi ya Akonaay imeweka wazi kwamba haki ya kumiliki ardhi chini ya mila na desturi ni mali inayolindwa na ibara ya 24 ya Katiba na kwa kuwa kauli ya Mahakama ya Rufaa ni kauli ya mwisho, basi ardhi ya jamii ya wafugaji wanaoishi na kutumia ardhi yao katika maeneo ya Loliondo na Ngorongoro kwa malisho, haiwezi kutwaaliwa na serikali bila kufuata taratibu za sheria zilizowekwa katika Sheria ya Utwaaji wa Ardhi, sura 118 (Land Acquisition Act). Mwenye mamlaka kutwaaa ardhi ni Rais na hanabudi afuate hatua zote za kutwaa ardhi zilizotajwa katika Sheria, sura 118. Kinyume na hii, uhamishaji wa wenyeji kutoka maeneo haya, kwa kulazimishwa au kwa hiari, ni batili na moja kwa moja inavunja sheria za nchi na haki za msingi za binadamu kama zilivyo orodheshwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa kuhitimisha barua yangu, Mheshemiwa, naomba nijumuishe hoja zangu kama ifuatavyo:

Mosi, ardhi yote ya Tanzania ni ardhi ya kiumma. Tamko hili la sheria ni tamko la kuainisha ardhi sio tamko la kumilikisha ardhi kwa serikali.

Pili, ardhi imewekwa mkononi mwa Rais kama dhamana. Kazi yake kama mdhamini ni kuhakikisha kwamba ardhi inawanufaisha wananchi na sio vinginevyo. Kisheria na kwa mujibu wa mila za kisheria tunazifuata, mdhamini (trustee) ana wadhifa wa kipekee na ni nzito. Uhusiano kati ya mdhamini na mnufaishwa ni uhusiano mahsusi ambao sheria na mila inaangalia kwa jicho la kipekee.

Tatu, umiliki ardhi wa moja kwa moja unabaki kwa wenye hati rasmi na watu au kaaya au jamii kwa mujibu wa mila na desturi.

Nne, umilikaji wa ardhi kupitia mila na desturi ni mali, property, na inalindwa na Katiba.

Tano, Ardhi ya mila haiwezi kutwaaliwa na Rais bila kufuata hatua zote zilizoainishwa katika Sheria ya Utwaaji wa Ardhi (Land Acquisition Act).

Mwisho, kutokana na mambo ya msingi niliyotaja hapo juu, wakaazi wa Ngorongoro na Loliondo, hususan jamii za wafugaji, hawawezi kuondolewa kutoka ardhi yao bila kufuata taratibu za kisheria na kwa sababu mahsusi ambayo lazima ijulikane na kujadiliwa hadharani.

Mheshemiwa Rais, sisi sote, wananchi pamoja na serikali tujiulize: Je, ondowaji wa wananchi kutoka ardhi yao, ambayo ni uhai na urithi wao, kwa minajili ya kupisha wanyama pori ili makampuni ya uwindaji, kwa mfano, yaweze kufanya shughuli zao kuwaleta wawindaji kuwinda wanyama pori bila kubughudiwa na wananchi, ni kwa manufaa mapana ya umma wa Tanzania? Nakiri sina jibu isipokuwa swali hili limenikosesha usingizi.

Nakutakia kila la kheri Mheshemiwa Rais

Issa Shivji

Profesa Stahiki (Professor Emeritus)

Shule Kuu ya Sheria

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Send this to a friend