Bashe: Upungufu wa sukari nchini utaisha Machi 2024

0
18

Kutokana na kuwepo kwa upungufu wa sukari nchini, Serikali imeeleza kuwa mvua za El Nino zinazoendelea kunyesha zimeathiri mfumo mzima wa uvunaji wa miwa na hivyo kuathiri wa uchakataji na kupelekea uwepo wa upungufu wa sukari.

Akizungumza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kutokana na mvua hizo, kiwango cha miwa kinachovunwa kimeshuka kwa wastani wa asilimia 25 hali iliyoathiri shughuli za uzalishaji na kupelekea upungufu ulioleta athari kwenye soko.

“Mchakato wa uvunaji wa miwa huvunwa kwa mashine maalumu kutoka mashambani. Mvua zilivyokuwa nyingi zimeathiri mfumo mzima wa uvunaji, na hivyo kuathiri mfumo mzima wa uchakataji kiwanda kama Kilombero ambacho kilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani 700 kwa siku, sasa kinazalisha tani 250, Kagera Sugar kilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani 500 kwa siku sasa kinazalisha wastani wa tani 200 mpaka 300,” ameeleza.

Aidha, amesema kiwango cha mahitaji ya sukari nchini kwa siku ni tani 1,500 lakini upungufu uliopo umepelekea uwezo wa viwanda kushuka na kuzalisha mpaka tani 1000.

Kutokana na hali hiyo, Serikali imesema hatua ya kwanza iliyochukua ni kuruhusu uagizaji wa sukari wastani wa tani laki 1 ambao umepewa viwanda nchini pamoja na kuwaagiza wenye viwanda na wasambazaji kuhakikisha wanasimamia usambazaji bila kumuumiza mlaji.

“Nataka niwaombe Watanzania wenzangu katika eneo hili la sukari tunaamini tutarudi kwenye hali yetu ya kawaida itakapofikia katikati ya mwezi Februari […] Hili ni jambo la mpito ni jambo ambalo litatuathiri kwa kipindi kisichozidi siku 30 na ninaamini baada ya hapo tutarudi katika stability yetu ya kawaida,” ameongeza.