Bashungwa awasimamisha kazi watumishi 5, awakabidhi TAKUKURU

0
72

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa ameagiza kusimamishwa kazi na kuhojiwa na Taasisi Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) watumishi watano kutokana kuisababishia hasara Halmashauri ya Wilaya Kiteto mkoani Manyara.

Watumishi hao ni aliyekuwa Mweka Hazina, Nassoro Mkwanda, Mhasibu wa Mapato, Christopher Mwigani, Kaimu Mwanasheria wa Halmashauri, Joseph Hoza, Kaimu Mweka Hazina Hadija Boffu pamoja na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi Nakaji Mollel.

Kati ya hao Nassoro Mkwanda aliyehamishiwa Mafinga Mji, Khadija Bofu aliyehamishiwa Songea Manispaa na Christopher Mwigani ambaye amestaafu wote wanatuhumia kuhamisha fedha na kuweka kwenye akaunti ya amana isiyo na vifungu vya matumuzi na wanatakiwa kurejeshwa kwenye halmashauri hiyo kujibu tuhuma hizo.

Pia, Kaimu Mkuu wa kitengo cha manunuzi Nakaji Melateki Mollel ambaye aliidhinisha TSh. milioni 191.9 kwa ajili ya kununua vifaa vya ujenzi bila kufuata taratibu sambamba na TSh. milioni 235.5 alizolipa mkandarasi wa kuchimbia visima bila kuzifanyia tathmini na Khalfan Hinga aliyetoa kazi hiyo bila kufanyika tathmini.

Amekemea tabia ya kuwahamisha watumishi waliofanya vibaya kwenye halmashauri na kusisitiza kuwa atawafuata popote walipo.

Kwa mujibu wa taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) 2019/20 na ile ya mwaka 2020/21 imeelekeza watumishi hao kuchukuliwa hatua kutokana na makosa hayo.

Pia, Bashungwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere kuhakikisha wanaodaiwa kiasi cha TSh. milioni 224.5 ambazo zilioneshwa kukusanywa lakini hazikufika benki kuwa wamerudishwa sambamba na kupiga mnada mali za mtumishi ambaye hakupeleka fedha benki ili kufikia fedha za Serikali.

Aidha, Bashungwa alisema kuna haja ya kuhoji Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri pale panapokuwa na ubadhilifu wa fedha kwa sababu ndio wanaohusika usimamizi.

Taarifa ya CAG imeonesha halmashauri hiyo ilikosa mapato takribani TSh. milioni 177.3 ambazo halmashauri ingezipata endapo wangehuisha leseni za biashara kwa mujibu wa taratibu.

Send this to a friend