Bashungwa: Kupasuka kwa barabara Basunzu siyo kosa la mkandarasi

0
18

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema uchunguzi uliofanywa umebaini mpasuko wa ardhi na kuporomoka kwa tuta la barabara uliojitokeza katika eneo la Busunzu lenye urefu wa mita 200 haijatokana na makosa ya mkandarasi kwenye ujenzi bali umesababishwa na sababu za kigeolojia.

Amebainisha kuwa kipande cha barabara hiyo kipo katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Manyovu – Kasulu – Kibondo – Kabingo awamu ya tatu ya barabara ya Mvugwe hadi Makutano ya Nduta (km 59.35) ambayo ilikwishakamilika kujengwa kwa kiwango cha lami.

Ametoa taarifa hiyo mkoani Kigoma leo Julai 10, 2024 mara baada ya kukagua eneo hilo na kupokea taarifa ya uchunguzi iliyofanywa na wataalamu wa miamba kutoka Taasisi ya Geolojia na utafiti wa madini Tanzania (GST), Kitengo maalum cha Utafiti cha TANROADS, na School of Mines and Geosciences (SoMG) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Nimepokea taarifa za kitaalamu na nimejionea zaidi ya mita 200 namna ambavyo majanga ya asili yalivyoathiri eneo hili, Serikali iliunda jopo la kufanya utafiti wa kina kuanzia mwezi Februari na tulichokigundua hapa sio makosa ya Mhandisi, sio upigaji kama watu wengine walivyodhani”, amesema Bashungwa.

Bashungwa ameitaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuendelea kutekeleza ushauri uliotolewa na wataalamu hao waliofanya uchunguzi huku akielekeza TANROADS kuhakikikisha wanafanya usanifu wa barabara kwenye maeneo korofi wakati wa mvua kwa kushirikiana na wataalamu wa miamba ili kubaini tabia za maeneo hayo na kuepuka changamoto zinazojitokeza.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta amesema baada ya taarifa za wataalamu wa miamba wameshauri kurudisha barabara sehemu ile ile iliyokuwa imejengwa awali ikiwa ni pamoja na kujenga upya tuta la barabara la mita 270 pamoja na kujenga surface na subsurface drainage ili kuruhusu maji yapite bila kuathiri tuta la barabara.

Send this to a friend