Bei ya mafuta kuendelea kupanda kwa miezi miwili

0
47

Kamishna wa Gesi na Petroli, Michael Mjinja amesema bei ya mafuta ya petroli nchini inatarajiwa kuendelea kupanda kwa kipindi cha miezi miwili ijayo kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo katika soko la dunia.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni nchini, Mjinja ameeleza kuwa kuna sehemu ya mgawanyo katika soko la dunia imeondolewa, na hiyo iliyobaki inagombaniwa na mataifa yote yanayoagiza mafuta hayo duniani.

“Sehemu ya mgawanyo kutoka Urusi imeondolewa katika soko la dunia na hiyo iliyobaki inagombaniwa, ndiyo sababu bei imepanda. Kwa sasa pipa moja la mafuta ghafi linagharimu dola za Marekani 100 hadi 105 (sawa na shilingi za Kitanzania 232,200 hadi 243,810) kutoka dola 70 za awali,” amefafanua.

Aidha ameongeza kuwa Tanzania inatumia mfumo wa uagizaji wa pamoja ambao una lengo la kuhakikisha upatikanaji wa petroli nchini unakuwa ni mkubwa sambamba na kuhakikisha ubora wa bidhaa hiyo.

Hata hivyo amesisitiza kuwa iwapo mgogoro wa Urusi na Ukraine utaendelea, bei ya mafuta itaendelea kubaki ilipo au kuendelea kupanda zaidi.

Send this to a friend