Bei ya Mafuta: Serikali kupunguza tozo na kubadili mfumo wa uagizaji mafuta
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kutafuta njia mbadala ambazo zitapunguza gharama ya maisha kwa Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
“Nawaomba Watanzania waendelee kuwa watulivu na waiamini Serikali yao kuwa tunaendelea kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha tunapunguza gharama za maisha kwa wananchi,” amesema.
Waziri Mkuu amesema huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameagiza viongozi wa sekta husika wahakikishe wanatafuta suluhisho la muda mfupi na muda mrefu la kupanda kwa bei ya mafuta hata kama bei hiyo inaendelea kupanda duniani.
Waziri Mkuu amesema kuwa tayari Wizara ya Nishati imeanza kutafuta njia mbadala za uagizaji wa mafuta pamoja na kupunguza makato mengineyo ili kupunguza bei ya mafuta.
“Serikali inaangalia njia mbadala za uagizaji wa mafuta, kupitia kwa wazabuni wengine kama ambavyo imeshauriwa na wabunge na tayari mchakato huo umeanza, kwa kutathmini maombi 24 ambayo yaliwasilishwa kwa Wizara na sasa wamebaki wazabuni sita ambao wameingia hatua inayofuata. Inachokifanya Serikali hivi sasa ni kujiridhisha na uwezo wao wa kusambaza mafuta kulingana na mahitaji na taratibu zilizowekwa na Serikali,” amesema.