Benki Kuu: Pato la Tanzania limekua kwa kiwango cha kuridhisha

0
40

Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya Benki Kuu imebaini kuwa Pato la Taifa kwa Tanzania Bara limekua kwa kiwango cha kuridhisha cha asilimia 5.4 na asilimia 5.2 katika robo ya kwanza na ya pili huku kukiwa na matarajio ya kufikia makadirio ya ukuaji wa asilimia 5.3 kwa mwaka 2023.

Kwa upande wa Zanzibar ulikua kwa asilimian 6.2 katika robo ya kwanza ya 2023, ambapo kuna uwezekano mkubwa wa kufikiwa kwa lengo la ukuaji wa asilimia 7.1 kwa mwaka huu.

Takwimu hizo ni matokeo ya mkutano wake wa 228 uliofanywa na kamati hiyo Oktoba 27, mwaka huu ili kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha, mwenendo na mwelekeo wa uchumi nchini.

Aidha, kamati hiyo imebaini kuwa mfumuko wa bei kwa Tanzania Bara umepungua na kufikia asilimia 3.3 kwa mwezi Septemba 2023 kutoka asilimia 3.6 mwezi Juni mwaka huu ukichangiwa na kupungua kwa bei za vyakula.

Hata hivyo, kamati imebaini kuwa uchumi wa dunia bado haujaimarika licha ya ukuaji wa juu ya matarajio uliofikiwa katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka.

Tanzania yashika nafasi ya 4 Afrika kwenye usalama wa anga

“Mwenendo huu unatokana na kubanwa kwa sera ya fedha katika nchi nyingi duniani, migogoro ya kisiasa na ongezeko la bei za mafuta. Mfumuko wa bei umepungua kutoka viwango vilivyofikiwa mwaka 2022, licha ya kubakia juu ya malengo kwa nchi nyingi, “ imeeleza taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha.

Kamati pia imebaini akiba ya fedha za kigeni imeendelea kubaki katika viwango vya kuridhisha vya takribani dola za Kimarekani bilioni 5 katika kipindi cha mwezi Julai mpaka Oktoba 2023, “kiwango kinachotosha kugharamia uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi, juu ya viwango vya nchi na jumuiya ya Afrika Mashariki vya miezi 4 na 4.5 mtawalia.”

Send this to a friend