Benki Kuu yakanusha kuchapisha fedha kwa ajili ya uchaguzi

0
95

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa inachapisha na kusambaza fedha kwa ajili ya uchaguzi mkuu, huku zingine zikihamasisha wananchi kuondoa fedha zao kwenye benki kwa madai kuwa baadhi ya benki zimeishiwa fedha kutokana na uchaguzi.

Taarifa ya Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Tutuba, imeeleza kuwa BoT huchapisha fedha kwa mujibu wa Kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu, Sura ya 197, na kuziingiza kwenye mzunguko kulingana na shughuli za kiuchumi na mahitaji ya kubadilisha fedha chakavu, na siyo vinginevyo.

“Napenda kuwathibitishia kuwa benki zote zilizopo nchini zinasimamiwa kwa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na vigezo vya kimataifa ambapo zimeendelea kuwa na mahitaji ya kutosha, ukwasi wa kutosha, zinatengeneza faida, na zina kiwango kidogo cha mikopo chechefu (asilimia 3.3 Septemba 2025) ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 5.0,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, BoT imewataka wananchi kutojihusisha na desturi ya kuondoa fedha benki na kuzihifadhi majumbani, ikisisitiza kuwa huo ni utamaduni wa kizamani unaohatarisha usalama wa fedha kwa sababu unaweza kusababisha wizi, uharibifu au matumizi mabaya.

Benki Kuu pia imeonya watu wote wanaosambaza taarifa za upotoshaji mtandaoni, ikisema vitendo hivyo havina tija kwa maendeleo ya sekta ya fedha na uchumi wa taifa.

Send this to a friend