Benki ya Dunia yapunguza makadirio ukuaji wa uchumi wa Kenya 2024

0
6

Benki ya Dunia imepunguza makadirio ya ukuaji wa uchumi wa Kenya kwa mwaka 2024 hadi asilimia 4.7 kutoka asilimia 5.0 ya awali, ikitaja athari za mafuriko, maandamano ya kuipinga serikali na juhudi za kuimarisha fedha.

Benki hiyo imesema Kenya imefanikiwa kuimarisha kiwango chake cha ubadilishaji wa fedha za kigeni, kuongeza akiba ya fedha taslimu katika benki kuu na kupunguza mfumuko wa bei mwaka huu, lakini bado inakabiliwa na hatari kubwa ya kukumbwa na madeni.

“Udhaifu wa madeni ikiwa ni pamoja na gharama za juu za kulipa madeni, na ukosefu wa malengo ya mapato bado ni changamoto kubwa,” benki hiyo ilisema katika ripoti kuhusu uchumi wa Kenya, ambayo kwa kawaida huchapishwa mara mbili kwa mwaka.

Imeongeza kuwa ingawa makadirio ya ukuaji wa mwaka huu ni ya chini kuliko kiwango cha mwaka jana cha asilimia 5.6, bado yatakuwa juu ya wastani wa asilimia 3.0 kwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Aidha, Benki hiyo imesema ukuaji wa Kenya utaongezeka hadi asilimia 5.1 katika robo ya pili ya mwaka ikiwa serikali itashughulikia kwa mafanikio changamoto za kifedha.

Maandamano yenye ghasia mnamo Juni yalimlazimisha Rais William Ruto kuachana na ongezeko la kodi lililolenga kukusanya zaidi ya dola bilioni 2 za mapato ya ziada, hali ambayo ilidhoofisha imani ya wawekezaji.

Send this to a friend