Benki ya Dunia (WB) kuikopesha Tanzania shilingi 3.9 trilioni

0
33

Benki ya Dunia (WB) imeihakikishia serikali ya Tanzania kuwa iko tayari kutoa fedha zote za mkopo wa masharti nafuu kiasi cha dola za marekani bilioni 1.7 (TZS 3.9 trilioni) zilizobaki katika mgao wa 18 wa Chama cha Kimataifa cha Maendeleo (IDA) ambacho hujihusisha na kuzisaidia nchi masikini zaidi duniani kupambana na umasikini.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo anayesimamia nchi 22 zilizoko Kanda ya Afrika, Bi. Anne Kabagambe wakati wa mazungumzo kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, yaliyofanyika Jijini Dar es salaam.

Alisema kuwa kiasi hicho cha fedha kinatarajiwa kutolewa kabla ya kuanza mgao mpya wa 19 wa IDA utakaoanza Julai 2020, baada ya kukamilisha taratibu zote za upatikanaji wa fedha hizo.

”Fedha hizi zitaelekezwa katika kutekeleza miradi kadhaa muhimu ikiwemo ya Elimu, Afya, Mradi wa kusaidia Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF, Awamu ya Pili na Uendelezaji wa Miji na Masuala ya Uchumi Jumuishi Visiwani Zanzibar” alisema Bi. Kabagambe

Waziri Dkt. Mpango ameiomba benki hiyo kuisaidia Serikali kwa kuipatia fedha za kufanikisha ujenzi wa miundombinu hiyo ya umeme, reli, maji safi na salama, kuimarisha sekta ya kilimo, viwanda, bandari, rasilimali watu na masuala ya teknolojia ya habari na Mawasiliano-TEHAMA.

Alibainisha kuwa miradi hiyo itachochea zaidi ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini wa wananchi kwa kuwa nishati ya umeme itachochea ukuaji wa sekta ya viwanda hivyo na kukuza ajira, wakati reli imara na ya kisasa itaimarisha mtandao wa reli na kuwa uti wa mgongo wa maendeleo ya Tanzania na nchi za Ukanda wa Afrika kwa ujumla.

Mpaka sasa, Benki ya Dunia imefadhili miradi 28 ya Maendeleo nchini Tanzania yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 5.0 sawa na takriban sh. trilioni 11.5, ambapo miradi 20 ni ya kitaifa yenye thamani ya dola 4.065 bilioni na miradi 8 ni ya kikanda yenye jumla ya dola za Marekani 938 milioni.

Send this to a friend