Benki ya Dunia imeahidi kutoa kiasi cha takribani Dola za Marekani milioni 300 [TZS bilioni 786.3] kwa ajili ya kusaidia Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini Tanzania, chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) ambayo inatarajiwa kutekelezwa baada ya kukamilika kwa Awamu ya Pili ya Mpango huo mwakani.
Hayo yameelezwa na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini, Nathan Belete katika majadiliano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo kuhusu mustakabali wa Awamu ya Tatu ya Mpango wa TASAF, yaliyofanyika Dar es Salaam.
Belete ameipongeza Serikali kwa mafanikio mbalimbali iliyoyapata kupitia Awamu ya Kwanza na ya Pili ya Mpango wa TASAF, na kuahidi kuwa benki hiyo kwa kushirikiana na washirika wengine wa maendeleo wataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha inafikia malengo yake hususan ya kuwawezesha wananchi kukabiliana na umaskini.
Naye, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) ambaye ameongoza majadiliano hayo, amesema Awamu ya Tatu ya Mpango wa TASAF itakuwa na mpango jumuishi utakaoendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa inayoandaliwa ya 2025 -2050.
“Uandaaji wa Mpango wa Tatu wa TASAF utahusisha shughuli za uzalishaji ambazo hazitabagua sehemu ya jamii yetu, makundi yote yatahusishwa katika shughuli za maendeleo na mgawanyo wa bajeti kwa ajili ya maendeleo hayo,” amesema Dkt. Nchemba.
Aidha, amesema Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya masikini inaandaliwa baada ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Mpango wa kwanza na wa pili, ambapo kumekuwa na shuhuda mbalimbali kutoka kwa wanufaika ambao vipato vyao vimeongezeka kutoka hatua moja kwenda nyengine.