Benki ya Dunia imeipongeza Tanzania kwa kuwa kinara na mfano wa utekelezaji bora wa programu ya uendelevu wa huduma ya maji na usafi wa mazingira vijijini Mashariki na Kusini mwa Afrika na Duniani inayotekelezwa kwa kutumia utaratibu wa malipo kwa matokeo, yaani Programme for Results (PforR), na kufadhiliwa na Benki ya Dunia ikijumuisha nchi zaidi ya 50.
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dkt. Victoria Kwakwa katika mazungumzo yake na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso nchini Ethiopia, amesifu mafanikio ya Tanzania ambapo zaidi ya miradi ya maji 1,500 imekamilika na inatoa huduma kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Kwakwa, Tanzania ilipokea awali Dola za Kimarekani milioni 350 [TZS bilioni 874.3] katika kipindi cha miaka mitano na ndani ya miaka mitatu ya kwanza, nchi ilifanikiwa kufikisha maji kwa zaidi ya watu millioni 4.7 vijijini, katika mikoa 17, ambapo mafanikio hayo yalisababisha Benki ya Dunia kuongeza ufadhili kwa Tanzania kwa dola za Marekani milioni 300 [TZS bilioni 749.4] na hivyo kuongeza wigo wa utekelezaji hadi mikoa 25.
Wizara ya Maji imebainisha kwamba mafanikio hayo yamefungua milango ya uendelevu wa programu hiyo hadi Julai 2025 na kutokana na mchango mzuri wa Tanzania, Benki ya Dunia imeonesha utayari wa kuendelea na PforR Awamu ya Pili kuanzia 2025 hadi 2030.