Benki ya Dunia yaipongeza Tanzania kwa usimamizi mzuri wa uchumi

0
12

Benki ya Dunia (WB) imeimwagia sifa Tanzania kwa usimamizi mzuri wa uchumi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inapopata fedha kutoka kwenye taasisi hiyo ikilinganishwa na nchi nyingine nyingi za Afrika.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika (Africa Group 1 Constituency), Dkt. Floribert Ngaruko, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania, unaoongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kwenye Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Jijini Washington D.C, nchini Marekani.

Dkt. Ngaruko amesema Tanzania ni nchi ya mfano katika usimamizi wa sera za uchumi na fedha ambapo licha ya changamoto za UVIKO 19 na vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine, tathimini ya Benki hiyo inaonesha kuwa uchumi wa Tanzania uko imara ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika.

“Tanzania ni nchi ya kuigwa mfano kwa usimamizi mahili wa masuala ya uchumi mpana, si tu kwa nchi za Afrika Mashariki, bali kwa nchi za Afrika, ambapo kiwango cha ukuaji uchumi cha wastani wa asilimia 5.4 ni cha juu, na ninawapongeza sana” amesema Dkt. Ngaruko

Tanzania yashika nafasi ya 10 kwa mamilionea wengi wa dola

Aidha, amepongeza uhusiano imara uliopo kati ya Tanzania na Benki ya Dunia na kuahidi kuwa benki yake itaendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kukuza uchumi na kuwaondolea umasikini wananchi kwa kusaidia fedha zitakazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii pamoja na kutoa misaada ya kiufundi.

Kwa upande wake, Waziri Nchemba ameishukuru Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo kwa kuiidhinishia Tanzania dola za Marekani bilioni 1.635 [TZS trilioni 3.8] katika mzunguko wa 20 wa IDA (Julai 2022 – Juni 2025) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 6 ya maendeleo katika sekta mbalimbali inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi pamoja na kupunguza umasikini wa wananchi.

“Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi makini wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania, tunaahidi kuwa tutasimamia na tutatumia fedha hizo kwa umakini ili kufikia malengo yaliyokusudiwa” amesema Dkt. Nchemba

Send this to a friend