Benki ya Dunia yajadili juhudi za kufikisha umeme kwa watu milioni 300
Rais wa Benki ya Dunia, Ajay Banga amesema Mkutano wa Kimataifa wa Nishati unaendeleza kazi ya miezi kadhaa iliyopita, ambapo makubaliano ya nchi 12 kuhusu Nishati yaliundwa kwa lengo la kuhakikisha watu milioni 300 wanapata umeme kati ya milioni 600 wanaohitaji huduma hiyo.
Akizungumza katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati jijini Dar es Salaam, Banga ameeleza kuwa lengo hilo ni gumu lakini linawezekana kufikiwa kwa ushirikiano wa pande mbalimbali, huku akiongeza kuwa Benki ya Dunia tayari imewaunganisha watu milioni 100 na inalenga kuwafikia milioni 250 zaidi kwa kushirikiana na mashirika mengine.
“Tunataka kuwafikia watu milioni 300 kati ya milioni 600. Hilo siyo jambo dogo. Ni lengo gumu lakini linawezekana. Itachukua juhudi kubwa, na hapo awali changamoto kubwa imekuwa ni ukosefu wa ushirikiano wa pande zote kushiriki,” amesema.
Aidha, katika hatua nyingine Banga ameeleza umuhimu wa biashara ndogo na za kati pamoja na wakulima wadogo, ambao wanachangia asilimia 80 ya ajira duniani, akieleza kuwa ili biashara hizo zifanikiwe, zinahitaji mazingira bora ya kisheria na upatikanaji wa mtaji wa gharama nafuu.
Licha ya changamoto za upungufu wa mitaji, Banga ametoa mwito wa kuhusisha sekta binafsi katika kufanikisha malengo ya maendeleo, akisema kuwa sekta binafsi inaweza kutoa mtaji, teknolojia, na ubunifu unaohitajika ili kufanikisha miradi mbalimbali, kwani maendeleo hayawezi kufikiwa bila juhudi za pamoja.
Naye, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Akinumwi Adesina ameshauri wakuu wa nchi za Afrika kuongeza bajeti kutoka kwenye bajeti zao wenyewe ili kusaidia miundombinu, uzalishaji wa umeme, usafirishaji wa umeme na usambazaji wa umeme, kwani wao ndio watakaohakikisha kwamba wanafikia muunganisho wa mwisho ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata umeme.